Thursday, June 28, 2012

Raia wa Nigeria wahimizwa kupanga uzazi

Wanawake wa Nigeria Sokoni
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan anasema wakati umefika raia wake kupanga uzazi. Kiongozi huyo amesema kuna watoto wengi sana wanaozaliwa na ipo haja kuwepo na sheria ya kuwa na mpango wa uzazi.
Ameongeza watu wasio jua kusoma wala kuandika wameendelea kuwapata watoto wengi ambao wanashindwa kuwapa mahitaji muhimu ya maisha.Umoja wa Mataifa unakadiria idadi ya Nigeria kuongezeka kutoka milioni 160 hadi milioni 400 ifikapo mwaka 2050.
 
Nigeria inaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watu Afrika na juhudi za awali kuwashawishi wazazi kuwapata watoto wachache ziligonga mwamba.
Mwandishi wa BBC Will Ross amesema ongezeko la watu linapunguza raslimali hali inayotishia kuwepo na machafuko ya kushindania raslimali hususan arthi.
Rais Jonathan amesema ipo haja kuwepo na sheria ya kudhibiti idadi ya watoto wazazi wanaopata katika siku za usoni.
Amelitaka Baraza la Idadi ya watu kuanza kampeini ya kushawishi jamii umuhimu wa mpango wa uzazi.
Amesema japo suala hili ni nzito kutokana na misimamo ya kidini na kimila, ipo haja jamii kubadilisha mawazo kwamba watoto ni baraka kutoka kwa Mungu.

Waasi wa Tuareg watimuliwa Gao,Mali

waasi nchini Mali
waasi nchini Mali
Majeshi ya Kiislam yanayohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda yameteka mji muhimu wa Gao, kaskazini mwa Mali, baada ya siku moja ya mapigano makali dhidi ya mahasimu wao wa kikundi cha Tuareg.
Watu wapatao ishirini wameuawa.
Msemaji wa Tuareg amesema kiongozi wao wa kisiasa amejeruhiwa katika mapigano hayo siku ya Jumanne, na amepelekwa nchi jirani kwa matibabu.
Wakazi katika mji huo wamesema kuwa waasi wameteka majengo katika mji huo na kupeperusha bendera zenye rangi nyeusi.
Baada ya wiki kadhaa ya makubaliano ya mashaka katika mji wa Gao, na baada ya kushindwa kuungana, wapiganaji wa Tuareg wameripotiwa kuondolewa katika mji huo muhimu na waasi hao wanaotaka kuweka sheria za kiislamu, za sharia.

mapigano makali

Mapigano makali yalizuka jana asubuhi kati ya makundi hayo hasimu na kusababisha watu kujifungia majumbani mwao siku nzima.
Daktari mmoja katika hospitali mjini Gao, amesema kupitia laini ya simu, kwamba watu wengi waliojeruhiwa walikuwa wamejihami, lakini pia raia walijeruhiwa katika mapigano hayo.
Daktari huyo amesema kwamba raia wawili walifariki dunia kutokana na majeraha waliyopata.
Miili ya watu pia iliripotiwa kuonekana katika miji mingine ya nchi ya Mali.
Mji wa Gao uko kwenye ufuko wa mto na umezungukwa na eneo kubwa lililo wazi. Kwa upande wa kaskazini ni jangwa la Sahara.

Gao mji wa kibiashara

Lakini kwa miaka mingi mji huo ulikuwa eneo muhimu la biashara ya matunda, mboga na mchele.
Bado mji wa Gao ni muhimu kwa sababu ndio njia muhimu ya kuelekea Mali ya kusini na pia ya kwenda nchi jirani za Niger na Nigeria.
Ndio sababu haishangazi kwamba mji huo ulitajwa kama makao makuu ya muda ya jimbo lililojitangazia uhuru wake la Azawad, wakati waasi wa Tuareg walipotwaa eneo la kaskazini mwa Mali, mapema mwaka huu

Ufadhili wa silaha waleta vita S Sudan

Wanajeshi wa Sudan Kusini
Silaha kutoka China, Ukraine na Sudan zinachangia machafuko Sudan Kusini. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Amnesty International. Ripoti ya shirika hilo imesema raia wameendelea kuawa na kujeruhiwa kiholela kwenye makabiliano kati ya kundi moja la waasi na jeshi la Sudan Kusini.
Amnesty International inasema silaha kutoka Sudan, mabomu ya kutegwa arthini kutoka China na Vifaru vilivyoagizwa Ukraini zimeendelea kutumiwa nchini humo. Hakuna upande ambao umejibu madai ya ripoti hii.
Vifaru vya Jeshi la Sudan Kusini vilitolewa kwa lililokua kundi la SPLA kati ya mwaka 2007 na 2009 kutoka Ukraine na kupitishiwa Kenya.Shirika hilo linaendelea kusema ,kampuni za Ujerumani na Uingereza ndizo zilihusika na usafirishwaji wa silaha hizo.
Kutolewa kwa silaha hizo kulifanyika licha ya kuwepo mkataba wa amani wa mwaka 2005 pamoja na marufuku ya silaha iliyowekewa Sudan nzima.Ripoti ya Amnesty International imenukuu machafuko katika Kaunti ya Mayom Jimbo la Unity.
Imesema kulengwa kiholela kwa kambi za jeshi kumesababisha maafa na majeruhi wengi miongoni mwa raia kinyume na sheria ya kimataifa inayosimamia masuala ya kibinadamu.
Shirika hilo sasa linazitaka serikali kutouza silaha kwa nchi ambazo huenda zikazitumia kutekeleza dhuluma za kibinadamu.Mwandishi wa BBC mjini Khartoum amesema huenda ripoti hii ikazua utata japo shirika lingine linalotathmini utumizi wa silaha limetoa taarifa sawa na hio.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake mwezi Julai mwaka jana baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miongo miwili.Japo ilisalia na visima vingi vya mafuta Sudan Kusini imeendelea kutumia mabomba ya Sudan kusafirishia mafuta yake kwa soko la kimataifa.

Wednesday, June 27, 2012

mashushushu, madaktari, wana habari Dk.Ulimboka alipofikishwa Muhimbili

mashushushu, madaktari, wana habari Dk.Ulimboka alipofikishwa Muhimbili

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, ambaye anaongoza mgomo wa madaktari nchini Dk.Steven Ulimboka akiwa na majeraha baada ya kutekwa na kushambuliwa na watu wasio julikana na kutupwa msitu wa Mabwe Pande uliopo nje ya jiji la Dar es Salaam usiku wa kuakia leo.
Wauguzi na Madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wakilisukuma gari la wagonjwa lililombeba mpigania haki zao Dk. Ulimboka wakati akitolewa chumba cha X-ray akipelekwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).


Madaktari wakisaidia kumuingiza Dk.Ulimboka katika gari la wagonjwa namba T 151 AVD la Hospitali ya AAR.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati akitoa taarifa ya kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoratibu mgomo wa madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, Dar es Salaam jana.
Dk. Cathbert Mchalo wa Taasisi ya Mifupa ya Moi (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumpokea, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata kutokana na kipigo.
Ofisa wa Polisi akimzuia mpiga picha wa gazeti la Tanzania Daima, Francis Dande, asimpige picha wakati wakimuondoa askari mwenzao aliyeshambuliwa na madaktari akituhumiwa kukutwa akipiga simu ya kuwataarifu wenzake kuwa Dk. Ulimboka hakufa.

Mmoja wa wana usalama wa (wa pili ushoto), akizozana na madaktari baada ya kumbaini akijifanya ni mwandishi wa habari na kumuamuru kuondoka eneo hilo mara moja.
Mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wa pili kulia, akizozana na Askari Polisi waliofika hospitalini hapo wakidai wanatafuta redio yao ya mawasiliano iliyopotea wakati wa pilikapilika za kumpokea Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo wa madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, alipoletwa akiwa hoi kutokana na kipigo kutoka kwa watu waliomteka usiku wa kuamkia jana na kumtupa msitu wa Mabwepande.
Madaktari wakiwa wamepigwa butwaa nje ya viwanja vya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia tukio hilo.

Wauguzi wakiwa nje ya wodi ya Kibasila wakitafakari jambo kufuatia jambo hilo
Wauguzi wakiwa nje ya wodi ya Kibasila wakitafakari jambo kufuatia jambo hilo

Tuesday, June 26, 2012

Mahakama ya Misri yabatilisha sheria

Wanajeshi Misri
Mahakama ya Misri imebatilisha uwamuzi wa serikali kukubalia jeshi kuwakamata raia. Mahakama hiyo imetoa uwamuzi wake baada ya kupitia malalamishi ya makundi ya kibinadamu ambayo yamepinga agizo hilo lililopitishwa Juni 13.
Mahakama hiyo imekuwa ikisikiliza kesi za kisheria ikiwemo hatua ya kufutwa bunge pamoja na kuundwa kwa baraza la katiba lililoteuliwa na bunge kuandika katiba mpya.
Watawala wa kijeshi wametumia amri ya mahakama na sheria za katiba ya zamani kuzuia makundi ya kiisilamu kua na udhibiti wa madaraka ya taasisi kuu nchini ikiwemo bunge.
Amri ya wanajeshi kua na uwezo wa kuwakamata raia imelalamikiwa na wanasiasa sawa na asasi za jamii kwamba inatishia kurejeshwa kwa sheria ya dharura.
Sheria ya jeshi kuwakamata raia ilimalizika hapo mwezi Mei baada ya kuwepo nchini Misri kwa miongo kadhaa.
Serikali inaweza kukata rufaa dhidi ya uwamuzi wa mahakama hiyo

MWILI WA MAREHEMU WILLY EDWARD WAWASILI MUGUMU SARENGETI KWA MAZISHI

Jeneza lenye mwili wa marehemu Willy Edward likiingizwa ndani baada ya kuwasili nyumbani kwao Mugumu, wilayani Seerengeti jana usiku
Mdogo wa marehemu Willy Edward (kushoto) akilia huku akilakiwa na ndugu yake baada ya mwili wa marehemu Willy Edward kuwasili nyumbani kwao
Baba mkubwa wa marehemu Willy Edward, Emmanuel Ongiri, akilia kwa uchungu huku akiwa amelalia jeneza lenye mwili wa mwanawe ulipowasili nyumbani kwao Mugumu, Serengeti usiku
Baadhi ndugu wa marehemu Willy Edward wakiangua kilio baada mwili kuwasili nyumbani kwao Mugumu, Serengeti

Sudan Kusini imefikia ndoto yake?


 
Sudan Kusini inaadhimisha mwaka mmoja wa uhuru wake mwezi Julai baada ya taifa hilo kujiondoa kutoka Sudan hapo Julai Tisa mwaka wa 2011.
Baada ya vita vya miaka mingi raia wa Kusini walijawa na matumaini, kwamba uhuru wa eneo lao utatoa nafasi ya kumalizika kwa matatizo ya nchi yao.
Wakati wa uhuru wake, Sudan Kusini ilitajwa kama moja wa mataifa masikini zaidi Barani Afrika. Nchi hii inaongoza na idadi ya vifo vya wanawake waja wazito na watoto. Aidha idadi kubwa ya wanawake hawajui kosoma na wala kuandika.
Mwaka mmoja baadaye nini kimebadilika?
Mwaka mmoja wa uhuru,Sudan Kusini imejipata katika mzozo na jirani wake Sudan hali iliyotishia kuzuka upya kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kuna hoja kadhaa zinajitokeza wakati Sudan Kusini ikiadhimisha mwaka mmoja wa uhuru;
Je matarajio ya raia yameafikiwa au matumaini yaliyokuwepo siku ya uhuru yamedidimia?
Sudan Kusini inaweza kujinasua kutoka historia yake iliyokumbwa na ghasia?
Nini kitahakikishia mustakabali wa Sudan Kusini?
Ndio mjadala wa mwezi huu unaongazia Afrika ambapo BBC itakuwa mjini Juba ,Ijumaa Juni 29.

Mohammed Mursi kuunda serikali mpya

Mohammed Musri akifanya sala
Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri Mohammed Mursi, anaanza kuunda serikali mpya baada ya kuahidi kuwa kiongozi wa raia wote wa Misri.
Viongozi wa dunia wamempongeza Kiongozi huyo aliyeungwa mkono na mrengo wa Muslim Brotherhood baada ya kumshinda Waziri Mkuu wa zamani Ahmed Shafiq.
Bw Musri anatarajiwa kuapishwa rasmi hapo Juni 30, japo kuna hoja kuhusiana na madaraka gani anapata.
Watawala wa kijeshi wamedhibiti madaraka mengi anayopata Rais pamoja na kufuta bunge.
Kwenye hotuba yake ya ushindi, Mursi aliwahakikishia raia kuwahudumia wote bila kubagua.
Mohammed Mursi anaanza kuunda serikali ya kiraia lakini macho yote yanatazaman chaguo lake la Waziri Mkuu.
Mwandishi wa BBC Jon Leyne mjini Cairo amesema kuwepo na mazungumo na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Mohamed ElBaradei, ambaye atatuliza wasi wasi wa mrengo usiopendelea sheria za dini na vijana.
Mursi ameahudi kuwateuwa manaibu wake na mawaziri kutoka pande zote.

MAPOROMOKO YAHOFIWA KUUWA WENGI

Bududa, Uganda
Bududa, Uganda
Shughuli za uokozi zinatarajiwa kuanza tena leo asubuhi mashariki mwa Uganda ambako vijiji vitatu vilifunikwa na udongo kufuatia maporomoka ya udongo yaliyokumba eneo la Bududa.
Shirika la msalaba mwekundu nchini Uganda limesema kuwa zaidi ya watu kumi na wanane wamefariki dunia katika maporomoko hayo.
Zaidi ya nyumba kumi na tano zimezikwa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.
Shirika hilo limesema maafisa wake wanaendelea kuwatibu waliojeruhiwa katika mkasa huo, katika eneo hilo lenye rutuba la Bududa, linalokuza kahawa na lililopo karibu na mbuga ya wanyama ya mlima Elgon.

nyumba zimefunikwa futi16 chini

Mwandishi wa habari, Stephene Mulaa, aliyezuru eneo la tukio amesema kuwa, ''kufikia jana jioni hakuna mwili hata mmoja ulikuwa umepatikana, kwa sababu inakadiriwa kwamba miili ya watu na nyumba zilizofunikwa na udongo ziko zaidi ya futi kumi na sita kwenda chini''

serikali kuwasaidia walioathirika

Serikali ya Uganda inatarajiwa kutoa taarifa kamili kuhusu janga hilo baadaye hivi leo.
Lakini kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, serikali imesema kuwa,'' inafanya juu chini kuhakikisha kuwa familia zilizoathirika zinapata msaada wa kutosha''.
Waziri anayehusika na maswala ya majanga, Dr Steven Malinga, amenukuliwa katika taarifa akisema kuwa hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa.
Mwaka 2010, maporomoko mengine ya ardhi yalitokea katika wilaya hiyo ya Bududa, na kuwauza zaidi ya watu mia tatu.
Eneo hilo linazungukwa na miinuko pamoja na mabonde, kando kando ya mlima Elgon, na hupokea mvua kubwa katika msimu wa masika.
Serikali imewashauri wakazi katika maeneo hayo kuhamia maeneo salama lakini wengi wamekataa kufanya hivyo wakihofia kupoteza mashamba yao yenye rotuba.
                               KARIBU  KATIKA BLOG HII YA JAMII