Wednesday, August 22, 2012

MISS TANZANIA 2012 AREJEA NYUMBANI KUTOKA MISS WORLD CHINA

 





Mrembo Lisa Jensen ambaye ni Miss World Tanzania 2012 amerejea jijini Dar es Salaam leo akitokea nchini China alipokwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Dunia mwaka huu na kupokelewa na viongozi kadhaa wa Kamati ya Miss Tanzania akiwepo Mkurugenzi wa Kino International Agency waandaaji wa Miss Tanzania Hashim Lundenga (kulia) aliyefika uwanja wa ndege wa JNIA Dar es salaam kumpokea.
Lisa akizungumza na viongozi wa Kamati ya Miss Tanzania, kutoka kushoto, Katibu Mkuu, Bosco Majaliwa, Mrembo Amisa Hassan, Mkurugenzi Hashim Lundenga na Ofisa Habari wa Kamati, Haidan Rico
Lisa akila pozi ya picha na mmoja wa warembo waliofika kumpokea Amisa Hassan. Lisa alifanikiwa kuingia Robo fainali za Top Model na kumi bora ya Shindano la Multmedia Award

''Kaa kando'' Todd Akins aambiwa

 

Mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Republican , Mitt Romney, amemtaka mwanasiasa mwenzake wa chama hicho kujiondoa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa kiti cha Useneta baada ya kutoa matamshi yaliyozua utata kuhusu ubakaji.

Mwanasiasa wa bunge la Congress, Todd Akin
Todd Akin, ambaye ni mwanasiasa wa bunge la Congress alizua manung'uniko kwa kudai kuwa mwili wa mwanamke una uwezo wa kuzuia mimba katika baadhi ya matukio ya ubakaji.
Matamshi ya Todd Kin anayegombea kiti cha seneta nchini Marekani yalitolewa wakati wa mahojiano. Alikuwa akitetea msimamo wake dhidi ya utoaji mimba.
Alipoulizwa kuhusu kutoa mimba iwapo mwanamke atabakwa, Todd Kin alieleza kuwa katika ubakaji halali au kile alichokitaja kuwa 'legitimate rape' kuna uwezekano kwamba kibiolioia, mwili wa mwanamke utamzuia kupata mimba anapobakwa.
Matamshi yake yamezua hisia kali.
Mpinzani wake Mitt Romney amesema, ''Matamshi yake kuhusu ubakaji yanaudhi sana na siwezi nikatetea msimao wake au nikamtetea yeye''
Baadhi ya wenzake Todd Akin kutoka chama cha Republican wamemtaka kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha useneta.
Hiki ni kipindi kigumu kwa wana Republican ambao walikuwa wamejiandaa kuendeleza kampeni yao kwa kumshambulia rais Obama kwa jinsi uchumi ulivyozorota wakati wa uongozi wake. Badala yake sasa wamejikuta wakirushiana maneno kuhusu sera za kijamii.
Chama cha Democrats kimechukua fursa hiyo kushambulia Republicans kwa kuwataja kama watu ambao hawazingatii maslahi na hisia za wanawake.
Todd Akin ameomba msamaha kufuatia matamshi yake.
"Nilitumia maneno yasiofaa na ninaomba msamaha. Nina watoto wawili wa kike na nataka haki kutendeka, nina roho ya huruma kwa waathiriwa wa ubakaji na nawaombea. Ukweli ni kuwa, mtu anaweza akapata mimba kutokana na ubakaji. Ukweli ni kwamba, kuna waathiriwa wengi wa ubakaji. Makosa yangu ni kutumia maneno yasiofaa. Naomba msamaha wako. ''
Hata hivyo halitakuwa jambo la kushangaza iwapo atalazimika kujiondoa kwenye mbio za kuwania kiti cha useneta kwa sababu ya matamshi hayo.

Rais wa Liberia amsimamisha kazi mwanae

Ellen Johnson Sirleaf anashutumiwa kwa kuendeleza upendeleo wa kindugu
Ellen Johnson Sirleaf anashutumiwa kwa kuendeleza upendeleo wa kindugu
Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, amemsimamisha kazi mmoja wa watoto wake wa kiume kutoka ngazi ya unaibu gavana wa benki kuu ya nchi hiyo kwa kushindwa kuorodhesha mali zake katika tume ya kuzuia rushwa nchini humo.
Charles Sirleaf, ni miongoni mwa maafisa 46 waliosimamishwa kazi kwa kosa hilo.
Ni mmoja wa watoto wake watatu wa kiume aliowateua kushika vyeo vya juu kabisa baada ya kushinda muhula wa pili wa uchaguzi mwaka jana.
Wapinzani wa Bi Sirleaf wanamshutumu kwa kuendeleza upendeleo wa kindugu.
Rais huyo amemteua mtoto wake wa kiume Fumba kuwa mkuu idara ya usalama wa taifa, na kijana mwingine Robert kuwa mshauri mkuu na mwenyekiti wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali-NOCAL.

Utawala bora

Robert Sirleaf anayashitaki magazeti mawili nchini humo ya Independent na Analyst, na mwanasiasa wa upinzani Jefferson Kogie kwa kumkashifu kuwa amejinufaisha kifedha kutokana na vyeo alivyopewa.
Taarifa kutoka ofisi ya Bi Sirleaf imesema Charles Sirleaf na maafisa wengine 45 wataendelea kuwa wamesimamishwa kazi hadi hapo watakapoorodhesha mali zao kwa Tume ya Kuzuia Rushwa.
Maafisa wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na mkuu wa itifaki ya rais, David Anderson, Wakili mkuu na naibu waziri wa sheria Micah Wilkins Wright na naibu mkurugenzi mkuu wa utangazaji Ledgerhood Rennie.
Liberia
Liberia

Bi Sirleaf aliyeingia madarakani mwaka 2005 mwishoni mwa mgogoro wa vita Uliodumu miaka 14, amekuwa akiahidi mara kwa mara kupambana na rushwa na kustawisha utawala bora nchini Liberia.
Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka jana, muda mfupi baada ya kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine katika uchaguzi ulioghubikwa na tuhuma za udanganyifu katika zoezi la upigaji kura.
Rushwa bado inabakia kuwa kikwazo kikubwa nchini Liberia huku idadi kubwa ya watu wakiishi katika umasikini licha ya utajiri mkubwa wa madini nchini humo.
Mwezi Juni taasisi ya kimataifa ya Maafa-ICG, ilitoa ripoti kutahadharisha kuwa rushwa na upendeleo wa kindugu katika sekta mbalimbali vinaweza kuhatarisha demokrasia nchini humo.